Tamko la Mh. Naibu Waziri Wa Afya, Ndungulile Kuhusu Watoto Wanaoingia Kidato Cha Kwanza Mwaka 2018
Napenda kutumia fursa hii kutoa ujumbe kwa watoto wa Tanzania, wazazi, walezi na jamii kwa ujumla katika kipindi hiki cha ambacho watoto wetu wanajiandaa kujiunga na kidato cha Kwanza katika Shule za Sekondari kwa mwaka wa masomo 2018.
Aidha, nawapongeza watoto wote waliochaguliwa kujiunga na elimu ya Sekondari kwa mwaka huu. Hii ni fursa muhimu ya kupata haki ya msingi ya kuendelezwa na hivyo kuwajengea watoto msingi madhubuti wa maisha ya baadaye kwa kutoa elimu na kuwa na jamii iliuyobora.
Elimu kwa watoto ni moja ya njia bora za kupunguza umasikini. Kwa mujibu wa taarifa ya Benki ya Benki ya Dunia, kila mwaka wa elimu kwa mwanamke unaongeza thamani ya pato lake la baadaye kwa asilimia 15 na asilimia 11 kwa mwanaume.
Kadhalika, nafasi ya elimu kwa mtoto wa kike na wa kiume husaidia katika makuzi bora kimwili, kiakili, kiroho, kimaadili, na kijamii.
Hivyo, ni vyema wazazi, walezi na watoto wenyewe wafahamu kuwa kuwaendeleza watoto wetu ni njia bora ya kutatua chjangamoto mbalimbali za maisha kwa maendeleo ya jamii yetu.
Nawaasa watoto wote wa kike na wa kiume kuzingatia wajibu wao na kutumia ipasavyo fursa hii muhimu ya kujiendeleza. Nawataka watoto kujiepusha na vitendo viovu kama vile masuala ya ngono, vileo, madawa ya kulevya na matumizi mabaya ya simu za mkononi kwani vinaweza kuhatarisha afya, usalama na kuwapotosha kimaadili hivyo kuathiri haki yao ya kuendelezwa na kuzima ndoto za maisha yao ya baadaye.
Watoto wote wa kiume na wa kike watambue kuwa wao ni hazina ya pekee katika maendeleo ya familia, jamii na Taifa letu.
Aidha, napenda watoto wafahamu kuwa fursa ya elimu ambayo wameipata ni maandaliziu ya kuwawezesha kubeba dhamana ya kufikisha nchi yetu katika uchumi wa kati na wa viwanda kama ilivyoainishwa kwenye Dira ya Taifa ya Maendeleo (2025), Mpango wa taifa wa maendeleo ya Miaka Mitano (2016/17- 2020/21) na Sera ya Maendeleo ya Mtoto Tanzania (2008).
Kwa kuzingatia hayo, Serikali itahakikisha watoto wote wanaendelezwa hadi kidato cha Nne ikiwa ni jitihada ambazo zimeasisiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa John Pombe Magufuli. Kwa kutambua juhudi hizi za Serikali, iwe ni mwiko kwa mzazi kutompeleka mtoto kujiunga na elimu ya Sekondari kwa kisingizio chochote kile.
Natumia fursa hii pia kuwakumbusha Watanzania wote kuwa vitendo vya kufanya ngono, kuoa na kuwapa mimba wanafunzi havikubaliki na hivyo wenye tabia hizo waache mara moja. Ikumbukwe kuwa kumpa mimba mtoto au mwanafunzi ni kosa la kijinai na kwa yeyote atakayebainika kufanya hivyo ikumbukwe adhabu yake ni kifungo cha miaka 30.
Aidha, natoa rai kwa wananchi wote kuendelea kutoa taarifa kwa mamlaka husika za Serikali za mitaa, Kijiji, Kata, Wilaya na hata katika madawati ya jinsia na Watoto yaliyopo katika vituo vya Polisi pale watakapobaini mzazi au mlezi amefanya hila kuzuia Mtoto kupata haki yake ya kuendelezwa.
Ninawatakia Mwaka mpya wenye furaha na mafanikio watoto, wazazi na watoto wote wanaoanza masomo ya Sekondari kwa mwaka 2018 na pia wanaoendelea.
Mungu ibariki Tanzania, Mungu wabariki Watoto wa Tanzania.
Imetolewa na:
Mhe. Dkt. Faustine Ndungulile (Mb.)
NAIBU WAZIRI
03/01/2018
Tamko la Mh. Naibu Waziri Wa Afya, Ndungulile Kuhusu Watoto Wanaoingia Kidato Cha Kwanza Mwaka 2018
Reviewed by Unknown
on
Januari 03, 2018
Rating:
Hakuna maoni: