DC SHINYANGA AFUNGUA KIKAO CHA TAHOSA SHINYANGA, ATOA TAHADHARI KWA WAKUU WA SHULE
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine MatiroMatiro amewatahadharisha wakuu wa shule za sekondari wilayani humo kutothubutu kuchangisha pesa kwa wazazi na wanafunzi kwa ajili ya mitihani ya shule na shule kwani ni kwenda kinyume cha agizo la rais John Pombe Magufuli linalokataza michango shuleni.
Matiro ametoa tahadhari hiyo leo Jumatano Februari 7,2018katika kikao cha kwanza kwa mwaka 2018 cha Umoja wa wakuu wa shule za sekondari Tanzania (TAHOSA) halmashauri ya wilaya ya Shinyanga (Vijijini) kilichofanyika katika ukumbi wa Mwalimu House Mjini Shinyanga na kuhudhuriwa na wakuu wa shule 27 za sekondari zilizopo katika halmashauri hiyo.
Aidha aliwataka wakurugenzi wa halmashauri za wilaya kutumia mapato ya ndani na juhudi za wafadhili au wadau wa elimu kufanikisha mitihani ya wilaya badala ya kuchangisha wazazi na wanafunzi.
"Naomba mitihani mnayofanya ya Interschool Examination isihusishe michango yoyote kutoka kwa wazazi na wanafunzi, tukihusisha michango tunakuwa tumekwenda kinyume na kanuni, taratibu na matamko yanayotolewa na viongozi wetu”,alisisitiza .
"Hakikisheni pia pesa za serikali zinatumika kulingana na kanuni na utaratibu uliopangwa,zisipotumika vizuri maana yake mmeshindwa kufanya kazi mtawajibishwa”,alieleza.
Mkuu huyo wa wilaya aliwakumbusha kuwa wakuu wa shule ndiyo wasimamizi wakuu wa shule na mambo yanapoharibika wao ndiyo watakuwa wa kwanza kuchukuliwa hatua.
“Kwa mwongozo uliopo sasa mkuu wa shule ndiye mdhibiti ubora wa shule wa kwanza, yaani ubora wa shule unakutegemea wewe, ina maana shule yako ikiwa na matatizo msababishi ni wewe na mwalimu mwandamizi wa taaluma, tumieni vizuri vitabu vya mwongozo mlivyopewa, kiongozi cha mwalimu mkuu ili kujikita katika mazingira salama mnapotekeleza majukumu yenu", alisema Matiro.
Mkuu huyo wa wilaya pia aliwataka wakuu hao wa shule kusimamia nidhamu kwa walimu na wanafunzi na kudhibiti utoro shuleni.
Matiro aliwataka walimu kujituma katika kazi na kuzitaka mamlaka zinazohusika kuwachukulia hatua walimu ambao shule zao kila mara zimekuwa zikifanya vibaya katika matokeo ya mitihani.
“Mwalimu upo pale kila mwaka wanafunzi wanafeli, wanapata ziro, shule inakuwa ya mwisho halafu mnamuacha tu huyo mwalimu kwanini? tuna walimu wengine pelekeni wakajaribu Labda kuna tatizo linalosababisha hayo maana kuna mtu mwingine kapewa majukumu yanayomzidi uwezo, mwekeni pembeni aingie mwingine tuone mabadiliko”,aliongeza.
Matiro aliwakumbusha pia wakuu wa shule kuwajengea wanafunzi hulka ya kupenda michezo na kuwapatia elimu ya kujitegemea badala ya kuwapa elimu ya darasani pekee na
Kwa upande wake mwenyekiti wa wakuu wa shule za sekondari halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Leonard Laurent alisema pamoja na nia njema ya rais Magufuli kuzuia michango shuleni,jamii imelipokea agizo hilo tofauti ambapo wazazi na jamii kwa ujumla hawajishughulishi na chochote katika maendeleo ya shule.
“Jamii sasa haijishughulishi na chochote,hata pale walipokuwa wameshaazimia wao wenyewe kuchangia gharama za samani (viti na meza),chakula na miundo mbinu kupitia kamati walizounda wenyewe hawashiriki tena”,alieleza.
Aidha aliwaomba viongozi wa serikali kuzunguka kila kata ili kukutana viongozi wa kata na wenyeviti wa serikali za vijiji ili watoe fasiri sahihi juuu ya nafasi ya ushiriki wa jamii katika kuleta maendeleo ya shule zao.
Imeandikwa na Kadama Malunde - Malunde1 blog
DC SHINYANGA AFUNGUA KIKAO CHA TAHOSA SHINYANGA, ATOA TAHADHARI KWA WAKUU WA SHULE
Reviewed by Unknown
on
Februari 07, 2018
Rating:
Hakuna maoni: