7 wapoteza maisha Na 12 Kujeruhiwa
Wakati Jeshi la Polisi likiendelea kutoa tahadhari ya mara kwa mara kwa madereva kuwataka waongeze umakini hasa katika kipindi hiki cha kuelekea msimu wa sikukuu za mwisho wa mwaka.
Ajali mbaya ya mabasi la abiria ilitokea jana na kusababisha vifo vya watu saba huku wengine 12 wakijeruhiwa vibaya.
Kwa mujibu wa mashuhuda, saba waliofariki dunia ni wanaume watano akiwamo dereva wa Toyota Hiace aliyetajwa kwa jina la Hassan na wengine wakiwa ni mtoto mdogo na mwanamke anayedhaniwa kuwa ni wa mtoto aliyefariki dunia.
Tukio hilo lililotokea jana majira ya saa 11:00 alfajiri, ikiwa ni siku nne tu kabla ya siku ya sikukuu ya Krismasi, lilitokea katika Kijiji Cha Kabeba, Kata ya Mwakizega, Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma baada ya basi kubwa la abiria aina ya Scania la kampuni ya Saratonga (namba T384 BMG) kugongana uso kwa uso na basi dogo aina ya Toyota Hiace ‘kipanya’, lenye namba za usajili T237BCE.
Taarifa zilizothibitishwa na Polisi kupitia kwa Kaimu Kamanda wake mkoani humo, Sweatbert Njewike, abiria wote waliofariki dunia walikuwa katika basi dogo lililokuwa likisafiri kutoka Kigoma Mjini kwenda katika Kijiji cha Lilagala, Wilaya ya Uvinza mkoani humo.
Majeruhi walipelekwa kwenye Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Kigoma wakiwa ni wa kutoka mabasi yote mawili. Basi kubwa lilikuwa likitokea eneo la kijiji cha Lilagala kwenda Kigoma Mjini.
Kwa mujibu wa Kaimu Kamanda Njewike, uchunguzi kuhusiana na ajali hiyo bado unaendelea kabla hatua zaidi hazijachukuliwa.
Hata hivyo, kamanda huyo aliongeza kuwa taarifa za awali zinaonyesha kuwa chanzo ni uzembe na ubabe wa madereva wa magari hayo baada ya wote wawili kukataa kupeana nafasi ya kupita kwa zamu kwenye daraja jembamba katika eneo hilo na mwishowe kugongana uso kwa uso wakati kila mmoja akijaribu kupita kwa kasi.
Kutokana na ajali hiyo, Kamanda huyo aliwataka madereva mkoani humo kuzingatia sheria za barabarani ili kujiweka mbali na ajali zinazoepukika na pia kutumia busara kwa kupeana nafasi wakati wanapokatiza kwenye maeneo tata kama ya kwenye madaraja madogo na kona kali.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Kigoma, Maweni Kibaya, alisema jana kuwa waliwapokea watu waliojeruhiwa katika ajali hiyo na kwamba walikuwa wakiendelea kuwatibia huku baadhi yao wakiwa na majeraha makubwa katika sehemu mbalimbali za miili yao.
7 wapoteza maisha Na 12 Kujeruhiwa
Reviewed by Unknown
on
Desemba 21, 2017
Rating:
Hakuna maoni: