Mameya wa Ubungo, Temeke wadaiwa kukunjana mashati
Mameya wa Ubungo, Boniface Jacob na wa Temeke, Abdallah Chaurembo wanadaiwa kukunjana mashati wakati wa kuhesabu kura za uchaguzi wa naibu meya wa Jiji la Dar es Salaam.
Katika uchaguzi huo, aliyeibuka mshindi, Mussa Kafana wa CUF alifikishwa kupiga kura akiwa mgonjwa. Kutokana na hali yake, alipigiwa kura na mbunge wa Ubungo (Chadema), Saed Kubenea.
Ilishuhudiwa katika ukumbi wa mikutano wa Karimjee ulikofanyikia uchaguzi huo leo Jumatano Januari 3,2018 Chaurembo na Jacob wakikunjana mashati.
Vurugu inaelezwa ilitokea baada ya Chaurembo wa CCM kupinga kura mbili alizodai zilipigwa nje ya utaratibu. Picha za wawili hao zilisambaa mitandaoni zikiwaonyesha wanavyokunjana.
Hata hivyo, Jacob amekanusha madai ya kupigana akisema alikuwa analinda kura zilizotaka kuchukuliwa na Chaurembo jambo ambalo hakutaka litokee na alifanikiwa.
Jacob alisema Chaurembo alivamia meza ya kuhesabia kura akitaka kura kwa ajili ya kuziharibu.
“Si kweli kwamba tumepigana mimi nilikuwa wakala, wakati kazi ya kuhesabu kura ikiendelea Chaurembo akaona kura za Chadema zinaongezeka ikiwa na maana kuna watu wa CCM walitupigia kura,” amesema.
Jacob amesema, “Kuona hivyo akavamia meza akitaka kunipora zile kura lakini nilikuwa nimezishika vizuri hivyo hakuweza kuzichukua na alidhibitiwa, hivyo kazi ya kuhesabu kura iliendelea kama kawaida na ndiyo kama hivyo tumeshinda,” amesema Jacob.
Wakati akisema hayo, Chaurembo amesema, ‘’Utaratibu wa uchaguzi haukufuatwa, kuna kura mbili zilipigwa nje ya kiboksi ambazo maana yake zimeharibika, lakini nilipohoji tu huyo jamaa (Meya Jacob) kama mnavyomjua, akanishambulia.”
“Akanirukia, akanikaba shati na kunichania, mimi nilikuwa napinga kura hizo kujumuishwa kwa kuwa zilikuwa zimeharibika,” amesema.
Mameya wa Ubungo, Temeke wadaiwa kukunjana mashati
Reviewed by Unknown
on
Januari 03, 2018
Rating:
Hakuna maoni: