Wanaokopa Matrilioni Nje Ya Nchi Kwa Dhamana ya Ardhi ya Tanzania Kubanwa Zaidi
Bunge
limesema limebaini ardhi ya Tanzania imewekwa dhamana ya mkopo katika
benki za ughaibuni na baadhi ya Watanzania na raia wa kigeni waliokopa
matrilioni ya shilingi.
Hayo yalielezwa mwishoni mwa wiki na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, Mohamed Mchengerwa
Mchengerwa
alisema kamati yake, mbali na mambo mengine, imetaarifiwa na serikali
kuwa kuna Watanzania na Wakenya wachache wamekopa matrilioni ya shilingi
katika benki za ughaibuni wakiweka dhamana mashamba yaliyopo nchini.
Alisema changamoto hiyo ndiyo iliyoilazimu serikali kuwasilisha Muswada wa Marekebisho ya Sheria mbalimbali Na.5 wa Mwaka 2017 ambao umeigusa Sheria ya Ardhi,
ili kutunga sheria ambayo itaondoa mwanya huo, akidokeza kuwa Sheria ya
Ardhi iliyopo ina dosari ya kutokuwa na kipengele kinachodhibiti hali
hiyo.
Muswada
huo unaotarajiwa kusomwa kujadiliwa katika mkutano wa 10 wa Bunge la 11
unaoanza leo, ulisomwa kwa mara ya kwanza bungeni Novemba, mwaka jana,
wakati wa mkutano uliopita wa chombo hicho cha kutunga sheria.
Mchengerwa
alisema kamati yake ilipata wiki mbili kwa ajili ya uchambuzi wa
muswada huo na kubainisha kuwa wameuboresha kwa kiasi kikubwa.
"Kwa
historia na taarifa ambazo tumepewa, kuna Watanzania, wale wa juu
kidogo ambao wao wamekwenda kukopea mashamba yetu ambayo yako wazi.
Wamekwenda kukopa matrilioni ya shilingi nje ya Tanzania wakiweka
dhamana mashamba yetu, na mashamba haya yako wazi, hayajaendelezwa,"
alisema.
Mchengerwa
alisema zaidi: "Na tunaamini sheria hii tukiipitisha na kama mikopo
itakwenda kuboresha mashamba, naamini Tanzania tutapiga hatua kubwa sana
kwa sababu kama leo hii zaidi ya Sh. trilioni moja, trilioni mbili ziko
nje ya nchi au zimekopewa na watu katika mashamba makubwa ambayo
tunayaona yana miti, hayajaendelezwa kabisa, na aliyekopa alidhamiria
kwenda kujenga kiwanda kwenye eneo lilelile au kulima kilimo fulani na
hajakiendeleza, inamaanisha zile Sh. trilioni mbili zingeiingia Tanzania
na kile kilimo kingelikuwa na tija."
Mbunge
huyo wa Rufiji (CCM) alibainisha kuwa muswada huo ulipowafikia ulikuwa
unagusa watu wote, lakini wameuboresha kwa kuondoa kipengele kinachozuia
hata wananchi wa kawaida kukopa fedha benki kwa kuweka dhamana ya ardhi
wanayoimiliki.
Alisema kwa sheria mpya itakayotungwa, madhumuni ya mkopo kwa dhamana ya ardhi ndiyo yataamua mtu kupatiwa mkopo huo au la.
"Na
sheria hii inakwenda kuweka uzalendo wa Mtanzania. Nchi kwanza, eeh!
Ukikopa fedha kwa ajili ya kilimo, na mikopo hii inatolewa na benki za
nje ya nchi ndiyo maana nikakudokezea tu kwamba kuna Watanzania
wamekwenda kukopa nje ya nchi, tena mikopo mikubwa, lakini hawajaboresha
lolote katika ardhi ambayo wameikopea," alisema.
"Sheria
hii (mpya) ni nzuri, ni moja ya sheria za kizalendo ambayo itatungwa na
Bunge la Tanzania. Na huu ni mfululizo wa sheria nzuri kama ile ya
madini, inakwenda kulinda rasilimali ya nchi yetu.
"Labda nikwambie tu kwamba wapo Wakenya wamechukua mashamba yetu na kwenda kuyawekea dhamana kwenye benki zao za Kenya.
"Kwa
hiyo sheria hii inakwenda kusaidia japokuwa sheria ya sasa inasema hata
kama kuna ardhi unaimiliki, Wizara ya Ardhi inaweza kukunyang'anya.
Wapo Watanzania, wachache sana lakini, ambao wamechukua ardhi yetu na
kwenda kuikopea huko nje.
"Sitaki
kuongea 'in details' (kwa kina) kwa sababu ni mambo ya kamati, lakini
wapo Watanzania na wengine si Watanzania, mfano hao Wakenya, ambao
wameweka ardhi yetu kama dhamana nje ya nchi."
Alisema
muswada uliofanyiwa kazi na kamati yake utakuwa na sura tofauti na ule
uliowasilishwa na serikali kwa kuwa umefanyiwa uchambuzi mkubwa na
maeneo mengi yameboreshwa kwa makubaliano kati ya Bunge na serikali.
Alisema
kamati yake imeongeza baadhi ya vifungu katika maeneo ambayo
yalionekana kuwa na utata au kutotoa tafsiri ya maneno na pia
wamepunguza baadhi ya vifungu ambavyo vilionekana vikipitishwa kama
ilivyopendekezwa na serikali havitakuwa na maslahi kwa taifa.
"Kwanza
kabisa tumeboresha na kuondoa kipengele ambacho kinajumuisha ardhi yote
kwa 'security' ya dhamana. Wapo wananchi wetu ambao ardhi yao kule
vijijini ambao na maeneo mengine wasiingie katika sheria hii.
Tukaongeza kifungu ambacho kinawaondoa Watanzania wa kawaida," alisema na kuongeza:
"Kwa
hiyo, kimsingi marekebisho haya yanakwenda kuwabana wale watu wakubwa
ambao siyo miongoni mwetu sisi wa kawaida. Ni wafanyabiashara wakubwa,
wanaochukua ardhi yetu kama dhamana halafu hawaendi kufanya lolote.
"Unajua
unapokwenda kukopa benki kwenye ardhi yako, kama unakwenda kukopa kwa
ajili ya kilimo fulani, basi sheria hii inataka uende ukalime. Hata kama
si kwenye eneo lote, ulime sehemu tu halafu fedha uiwekeze maeneo
mengine. Sheria hii haizuii kwamba fedha yote iingie kwenye kilimo.
"Tunataka
tujiridhishe ile ardhi yako unaitumia kwa ajili ya kilimo? Umeendeleza
kilimo? Lakini kama unataka kukopa kwa vitu vingine, unataka kukopa kwa
ajili ya ujenzi wa ghorofa, madhumuni ya mkopo lazima yaonyeshwe kwenye
maombi yako unayokwenda kuiombea mkopo."
Wanaokopa Matrilioni Nje Ya Nchi Kwa Dhamana ya Ardhi ya Tanzania Kubanwa Zaidi
Reviewed by Unknown
on
Januari 29, 2018
Rating:
Hakuna maoni: