Kigwangalla Awatupia Tuhuma Nzito Lowassa na Sumaye
Waziri
wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla amesema vigogo watano ni
miongoni mwa wanaotajwa kuwa ni kati ya watu 83 waliochukua maeneo na
kujenga nyumba katika kiwanja cha Mamlaka ya Hifadhi Ngorongoro (NCAA),
wakiwamo mawaziri wakuu wa zamani, Edward Lowassa na Frederick Sumaye.
Akizungumza
na wajumbe wa bodi mpya ya NCAA aliyoizindua jana, Dk Kigwangalla
alisema mwingine ni Daniel Ole Njoolay ambaye aliwahi kuwa mkuu wa Mkoa
wa Arusha.
“Nimewataja
hawa baadhi, najua kuna wengine, sasa naipa jukumu bodi na menejimenti
kuendelea kuwataja na hatua za kurejesha ardhi zianze,” alisema.
Waziri huyo alisema tayari ameshamueleza Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi juu ya mgogoro huo.
Alisema
anajua njama zilizotumika kugawa eneo hilo la ekari 20 kati ya 40 kwa
kuwa jiji la Arusha lilikuwa halina uwezo wa kugawa eneo ambalo si lake.
“Jiji
wamegawa eneo hili mwaka 1996 wakati likiwa chini ya umiliki wa Shirika
la Taifa la Utalii lililobinafsishwa na NCAA walinunua hili eneo mwaka
2006,” alisema.
Lakini,
mmoja wa wakazi wa eneo hilo, Juliana Peter alisema walipata viwanja
hivyo baada ya jiji kutangaza kuvigawa wakifuata taratibu zote, “Mzazi
wangu ndiye alinunua kiwanja na najua ana hati hivyo sisi si wavamizi.”
Mbali
na kuitaka kufuatilia suala hilo la ardhi, Dk Kigwangalla ameitaka,
“kusaidia kusimamia mali za NCAA lakini pia kuongeza siku za watalii
kukaa Ngorongoro kutokana na kuongeza vivutio.”
“Pia
mnapaswa kukaa na jamii kuboresha mahusiano ili ule mpango wa
Ngorongoro wa miaka 10 ufanikiwe, hivyo mnapaswa kukaa na jamii kutafuta
namna bora ya kujenga mahusiano kupitia miradi ya maendeleo,” alisema.
Dk
Kigwangalla alirejea agizo lake kwa Jeshi la Polisi kutaka liwakamate
watuhumiwa wanne kwa madai ya kushiriki katika mtandao wa ujangili ndani
ya siku saba.
Alitoa
agizo hilo Januari 25 na kusisitiza kwamba jeshi hilo likishindwa
kuwakamata, atalishtaki kwa Amiri Jeshi Mkuu ambaye ni Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania.
Dk
Kigwangalla alisema jana kwamba anasubiri siku saba zifike na kama
hatua zitakuwa hazijachukuliwa atafikisha suala hilo kwa Rais John
Magufuli.
“Uamuzi
wangu niliotangaza Januari 25 upo palepale nilitoa siku saba hazijafika
ila zikifika kama hakuna hatua nitampelekea Rais jambo hili,” alisema.
Alisema ana imani kubwa na Polisi kuwa itazifanyia kazi taarifa alizotoa.
Hata
hivyo, siku moja baada ya kutoa agizo hilo, msemaji wa jeshi hilo,
Barnabas Mwakalukwa alisema halifanyi kazi kwa matamko, bali kwa kufuata
kanuni, taratibu na sheria za kuanzishwa kwake.
Kigwangalla Awatupia Tuhuma Nzito Lowassa na Sumaye
Reviewed by Unknown
on
Januari 29, 2018
Rating:
Hakuna maoni: