Polisi watakiwa kuweka mikakati endelevu ili kuboresha afya za wanaowahudumia
Wataalamu
wa afya wa Jeshi la Polisi wametakiwa kujiweka tayari katika kujadili
changamoto na kuibua mikakati endelevu ili waweze kuboresha huduma za
afya kwa watu wenye uhitaji, askari pamoja na familia zao.
Hayo
yamesemwa katika hoteli ya SG Resort iliyopo jijini hapa na Kamanda wa
Polisi mkoa wa Arusha Naibu Kamishna (DCP) Charles Mkumbo kwa niaba ya
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, wakati wa ufunguzi wa semina ya siku
mbili ya wakuu wa vituo tiba vya Polisi Tanzania pamoja na wafanyakazi
na watumishi wa JSI kuhusiana na uboreshaji utoaji wa huduma za afya
katika kukabiliana na jukumu la kupambana na uzuiaji wa maambukizi ya
VVU na UKIMWI.
Alitoa
wito kwa Madaktari, Wauguzi na watumishi wengine wanaofanya kazi katika
Zahanati na vituo vya afya kuendelea kuwatambua wenye maambukizi ya VVU
na UKIMWI kwa kuwapima, kuwaanzishia dawa na kuhakikisha wote walioanza
matibabu wanaendelea kutumia dawa kwa kipindi chote cha uhai wao.
Kamanda
Mkumbo aliendelea kuwakumbusha washiriki wa mkutano huo kuendelea
kuwahudumia wananchi kwa uadilifu na utunzaji mkubwa wa siri za wateja
wanaopatiwa huduma za VCT/CTC ikiwa ni sehemu ya kiapo chao juu ya
taaluma yao.
Naye
Mganga mkuu wa Kikosi cha Afya cha Jeshi la Polisi nchini Mrakibu
Mwandamizi wa Polisi (SSP) Charles Msenga, alisema kwamba lengo la
semina hiyo ambayo inawezeshwa na JSI/AIDS FREE ni kujitathmini namna ya
utoaji huduma bora kwa askari, familia zao pamoja na wananchi wengine
wanaotumia vituo hivyo.
Alisema
kwamba ubora wa huduma ambao wanatoa umekuwa ukiongezeka siku hadi siku
ambapo wataalamu hao wa afya wamekuwa wakihakikisha kwamba wagonjwa
wote wenye matatizo wanapatiwa dawa na walioacha dawa wanafuatiliwa na
kuendelea kuhudumiwa.
Alisema
vituo vyao vya Afya vimekuwa vikitoa Ushauri Nasaha na Kupima (VTC)
lakini pia kwa wagonjwa wamekuwa wakipata huduma za Uangalizi pamoja na
kupewa dawa (CTC) hali ambayo imesaidia watu wengi kujitokeza kupima na
kufahamu afya zao.
Awali
akizungumza katika Semina hiyo iliyojumuisha washiriki 50 kutoka vituo
mbalimbali vya afya vya Polisi nchini, Mkurugenzi wa AIDS FREE Dr.
William Nyagwa, alisema kwamba shirika hilo lisilo la kiserikali
linataka siku za usoni UKIMWI uwe historia na kuwataka wana semina hao
kuendelea kujitoa kufanya kazi hiyo huku akiwahakikishia kwamba wao wapo
nyuma yao.
Aidha
alitoa wito kwa askari pamoja na familia zao kujitokeza kwa wingi
kupata huduma kupitia vituo hivyo vya afya kwani kwa mgonjwa itakuwa
rahisi kuhudumiwa na kuwahakikishia kwamba wataalamu wanaotoa huduma
katika vituo vya afya wamekula kiapo hivyo wasiwe na wasiwasi juu ya
usiri.
Dr.
Nyagwa alisema Semina hiyo pia itatoa uhuru kwa washiriki wote kuelezea
changamoto zinazowakabili katika maeneo yao ya kazi ili ziweze
kutatuliwa.
Na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha
Polisi watakiwa kuweka mikakati endelevu ili kuboresha afya za wanaowahudumia
Reviewed by Unknown
on
Februari 08, 2018
Rating:
Hakuna maoni: