Gdobless Aibua Upya Sakata la Matibabu ya Tundu Lissu Bungeni
Mbunge
wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema amehoji sababu za Bunge
kutogharamia matibabu ya Tundu Lissu aliyepo nchini Ubelgiji tangu
Januari 7, 2018 akipatiwa tiba ya mazoezi.
Lema
ametoa kauli hiyo jana Februari 8, 2018 bungeni mjini Dodoma wakati
akichangia taarifa za utekelezaji wa shughuli za kamati za Bunge za
Utawala na Serikali za Mitaa, Katiba na Sheria na Sheria Ndogo.
Lissu
ambaye ni mbunge wa Singida Mashariki (Chadema) alishambuliwa kwa zaidi
ya risasi 30 akiwa ndani ya gari lililokuwa nje ya makazi yake mjini
Dodoma Septemba 7 mwaka jana, kupatiwa matibabu Hospitali ya Mkoa wa
Dodoma ambapo siku hiyo hiyo alihamishiwa Hospitali ya Nairobi, Kenya.
Alipelekwa
Ubelgiji Januari 7 kwa ajili ya tiba ya mazoezi na mara kadhaa familia
yake imelishutumu Bunge kuwa kimya kuhusu matibabu ya mbunge huyo ambaye
pia ni Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS).
Katika mchango wake, Lema alianza kwa kutoa pole kwa Spika wa Bunge, Job Ndugai aliyedai kuwa yupo nchini India kwa matibabu.
“Mheshimiwa
Spika anatumia fedha za Serikali kupata matibabu na mbunge Lissu
tumeendelea kumtafutia fedha za matibabu mitaani tena kwa mkopo,”alisema
Lema.
Alibainisha
kuwa kitendo cha Ndugai kutibiwa na fedha za Serikali huku Lissu ambaye
ni mnadhimu wa Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni akishindwa kupewa msaada
na Bunge ni jambo ambalo halikubaliki.
Wakati
akieleza hayo, alikatishwa na Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge
akimtaka ajielekeze kwenye hoja tatu za taarifa za kamati huku mbunge wa
Kishapu (CCM), Suleiman Nchambi akisema bima walizonazo wabunge
zinawawezesha kupata matibabu.
“Kama hawana mawasiliano mazuri na Bunge nawashauri na nawapa taarifa wawasiliane na ofisi ya Bunge,” alisema Nchambi.
Kauli
ya Nchambi iliibua mvutano bungeni, huku mbunge wa Tarime Vijijini
(Chadema), John Heche akisikika akisema kauli ya mbunge huyo wa Kishapu
ni sawa na kucheza na uhai wa mtu.
Kufuatia
hali hiyo, Chenge aliingilia kati na kuwatuliza wabunge hao kwa
kuwataja kwa majina, akiwemo Heche na mbunge wa Iringa Mjini (Chadema),
Mchungaji Peter Msigwa.
Mwenyekiti
huyo alipomtaka Lema kuendelea na mchango wake, mbunge huyo aliendelea
kuzungumzia matibabu ya Lissu na kubainisha kuwa suala hilo linahusu
utawala bora, si vinginevyo kama inavyodaiwa na Nchambi.
“…,
Huyu (Nchambi) anasimama anaongea mzaha kuna watu wamepotea mmoja
anaitwa Ben Saanane (msaidizi wa mwenyekiti wa Chadema-Freeman Mbowe)
haya ni mambo yanayohusu utawala bora na sheria,” alisema Lema.
Alisema kujadili matibabu ya Lissu na masuala ya utekaji hawana lengo la kushutumu, bali ni kutaka mambo yarejee katika mstari.
Licha
ya Lema kuendelea kuchangia taarifa hizo za kamati huku akikatishwa
mara kwa mara, muda wake ulipomalizika alitakiwa na Chenge kuketi ili
kumpisha mchangiaji mwingine.
Gdobless Aibua Upya Sakata la Matibabu ya Tundu Lissu Bungeni
Reviewed by Unknown
on
Februari 08, 2018
Rating:
Hakuna maoni: