Tanzania kuwa na watu 58 milioni ifikapo mwishoni mwa mwaka huu
Tanzania
inatarajiwa kufikisha idadi ya watu milioni 58 ifikapo mwishoni mwa
mwaka huu ikiwa ni ongezeko la juu ikilinganishwa na idadi ya awali ya
watu milioni 46 iliyoripotiwa mwaka 2010.
Kwa
mujibu wa Idara ya Jamii na Mambo ya Uchumi ya Shirika la Umoja wa
Mataifa (UN), makadirio hayo ni sawa na kila kilomita moja ya mraba kuna
wakazi 67 tofauti na makadirio ya mwaka 2010 ya watu 52.
“Tanzania
ina kiwango kikubwa cha kuzaliana duniani na zaidi ya asilimia 44 ya
watu ni chini ya miaka 15. Kiwango cha kuzaliana ni watoto 5.01 kwa
mwanamke mmoja ambacho ni kikubwa kwa nchi kama Tanzania,” ripoti hiyo
ya makadirio ya UN inaonyesha.
Inasema kila sekunde 14, mtoto mmoja anazaliwa nchini huku mtoto mmoja akifariki dunia kila baada ya sekunde moja.
Makadirio
hayo pia yanaonyesha kuwa idadi ya watu nchini imeongezeka kwa asilimia
3.15 kwa kipindi cha miaka minane iliyopita wakati kiwango cha
kuzaliana kilikuwa ni asilimia 5.17 kati ya mwaka 2015 na 2018.
Ikiwa
hali hiyo itaendelea hivyo, ripoti hiyo inabainisha kuwa kwamba idadi
ya watu itaongezeka kufikia milioni 95.5 ifikapo mwaka 2050 na watu
milioni 300 ifikapo mwaka 2099.
Mchanganuo
wa ripoti hiyo unaonyesha kuwa makadirio hayo ni sawa na asilimia 0.77
ya idadi ya watu duniani kwa mwaka huu kutoka asilimia 0.66 katika mwaka
2010.
Tanzania
imewekwa katika nafasi ya 24 miongoni mwa nchi zenye idadi kubwa ya
watu duniani mwaka huu, kiwango ambacho ni kikubwa ikilinganishwa na
mwaka 2010 ambapo ilikuwa nafasi ya 28.
Idadi
ya hivi sasa ya watu waishio mijini inakadiriwa kufikia milioni 19.2
sawa na asilimia 31 ya idadi ya watu wote ikilinganishwa na ile ya awali
ya mwaka 2010 iliyokuwa milioni 12.6 ambayo ilikuwa sawa na asilimia
27.4.
Hata
hivyo, kulingana na makadirio ya idadi ya watu nchini mwaka 2016-17
yaliyofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), ilikadiriwa kwamba
kungekuwa na idadi ya watu milioni 51.55 katika kipindi cha mwaka jana.
Tanzania kuwa na watu 58 milioni ifikapo mwishoni mwa mwaka huu
Reviewed by Unknown
on
Februari 08, 2018
Rating:
Hakuna maoni: